MAPIGANO makali kati ya wakulima na wafugaji yaliyozuka katika eneo la
Ikwiriri wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani na kusababisha vifo, majeruhi,
nyumba kuchomwa moto, maduka kuvunjwa na barabara kufungwa kwa zaidi ya
saa sita.
Chanzo cha mapigano hayo, kinaelezwa kuwa ni kutokana na
kuuawa mkulima wa Ikwiriri, Shamte Seif (60) na wafugaji katika ugomvi
uliotokana na ng’ombe kuingia kwenye shamba lake. Hadi jana jioni,
watu kumi na moja walikuwa wameripotiwa kujeruhiwa, tisa kati ya hao
wamelazwa katika Kituo cha Afya Ikwiriri na wawili walihamishiwa katika
Hospitali ya Misheni Mkuchu, Ikwiriri baada ya hali zao kuwa mbaya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alithibitisha kuuawa kwa Seif na kusema wafugaji wawili wanashikiliwa na polisi. Habari
zilizopatikana kutoka Ikwiriri zinasema, baada wananchi kupata taarifa
za kifo cha mkulima kisha kushiriki katika mazishi yake, ndipo
walipoanza kuwasaka wafugaji popote walipo. Bila kujali kama
walihusika au la katika mauaji hayo, wakulima hao wakiwa na silaha za
jadi ikiwemo mishale, walivamia nyumba kadhaa zinazodaiwa kuwa za
wafugaji na kuzichoma moto. Taarifa zinasema wakulima hao
waliungana na wananchi wengine kuwawinda wafugaji popote walipo kwa
lengo la kulipiza kisasi cha mauaji hayo. Aidha, walikwenda kwenye
Kituo cha Polisi Ikwiriri wakitaka wakabidhiwe watuhumiwa wa mauaji ya
mkulima huyo ili wawashughulikie. Katika vurugu hizo, kundi hilo la wapiganaji lilivunja duka la dawa lililopo Ikwiriri na kupora dawa zote zilizokuwemo. Pia
kundi hilo liliweka mawe na magogo kwenye Barabara Kuu itokayo Dar es
Salaam kwenda Mtwara na kusababisha magari kusimama kwa zaidi ya saa
sita. Wakati magari hayo yakiwa yamesimama, wapiganaji hao
walikuwa wakiyarushia mawe na kusababisha mengine kugeuza na kurudi
yalikotoka. Habari zinasema magari mengi yaliharibiwa vibaya
likiwemo moja la aina ya Toyota Noah hali iliyomlazimu mmiliki wake,
kupiga risasi takriban 10 hewani kwa lengo la kuwatawanya wapiganaji
hao, hali iliyosababisha eneo hilo kuwa kama uwanja wa vita. Baadhi ya wafugaji katika eneo hilo na maeneo ya jirani ilibidi watelekeze mifugo yao na kujificha kunusuru maisha yao. Vurugu hizo zilililazimu Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kuomba nguvu ya ziada kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo, Dar es Salaam. Helikopta moja na magari yaliyokuwa na Askari wa FFU zaidi ya 80 yalitolewa kwenda kuongeza nguvu. Taarifa zaidi kutoka Ikwiriri zinasema, vurugu hizo ni kubwa ambazo hazijawahi kutokea katika eneo hilo. Inadaiwa
kwamba katika siku za hivi karibuni kumekuwa na migogoro ya mara kwa
mara kati ya jamii hizo na kwamba wakulima wamekuwa wakikasirishwa na
vitendo vya wafugaji kupitisha mifugo kwenye mashamba yao. Migogoro hiyo imekuwa ikizidi pale mifugo hiyo ilipobainika kula mazao yao. Hata hivyo, wafugaji hao wanadaiwa kuwa wamekuwa wakiendelea kupitisha mifugo yao kwenye mashamba ya wananchi.
0 comments:
Post a Comment