Pages

Pages

Saturday, June 2, 2012

Nsajigwa atemwa Yanga

KLABU ya Yanga imewatupia virago beki wake wa kulia na nahodha, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ na Abuu Ubwa, imefahamika. Habari za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam zinasema, nyota hao wameachwa kutokana na kushuka viwango.
Chanzo cha uhakika kimedokeza kuwa kushuka kwao kiwango kuliwafanya washindwe kutoa mchango uliotarajiwa kutoka kwao katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyofikia tamati Mei 6. Yanga chini ya Kocha wake Mserbia, Kostadin Papic ilimaliza ligi hiyo kwa kushindwa kutetea ubingwa wake, ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC. Chanzo hicho kimedokeza kuwa, kuachwa kwa nyota hao, ni sehemu ya mkakati wa kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kuelekea vita ya kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame na msimu mpya wa Ligi Kuu.
Mbali ya kiwango, pia kiongozi huyo amedokeza kuwa, walikerwa na utovu wa nidhamu wa ndani na nje ya uwanja wa Nsajigwa aliyekuwa nahodha wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars. “Tumedhamiria kuwa na kikosi bora, sio bora kikosi kwenye ligi kuu ijayo na michuano mingine, hivyo hatuwezi kuwa na wachezaji walioshuka viwango,pia nidhamu mbovu,” alisema kiongozi huyo. Alidokeza kuwa, kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kusaka nyota bora ambao wataziba nafasi za wale watakaoachwa kwa lengo la kujenga kikosi bora cha ushindani. Mbali ya Nsajigwa na Ubwa, nyota wengine walio kwenye hatari ya kutemwa,ni Shamte Ally, Bakari Mbegu na Kiggi Makasy kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo kushuka viwango. Kuachwa kwa Nsajigwa kunakuja huku kukiwa na habari za Yanga kuanza kusaka saini za nyota kadhaa wakiwemo Uhuru Seleman, Juma Jabu na Juma Nyoso kwa lengo la kuimarisha kikosi cha msimu ujao. Shadrack, ni kati ya mabeki shupavu nchini akijaaliwa uwezo wa pumzi kiasi cha kupanda kwenda kusaidia mashambulizi na kushuka kuzuia, akifananishwa na lori aina ya Fuso ambalo hutumika kubeba mizigo. Kabla ya kutua Yanga mwaka 2006 akitokea timu ya Moro United, Nsajigwa aliwahi kuichezea Prisons ya Mbeya kwa mafanikio kama ilivyokuwa kwa rafiki yake, kipa Ivo Mapunda aliyehama naye Moro Utd hadi Yanga. Katika mechi ya mwisho ya kufunga Ligi Kuu dhidi ya Simba iliyopigwa Mei 6 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Nsajigwa alionekana kupwaya, akisababisha penalti tatu kutokana na kucheza rafu dhidi ya Emmanuel Okwi.

No comments:

Post a Comment