Pages
▼
Pages
▼
Friday, May 4, 2012
Basi la NBS lapata ajali mbaya-Tabora
Abiria
saba wamefariki dunia na wengine 54 wamejeruhiwa vibaya, baada ya basi
walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Arusha kupasuka tairi la
mbele na kisha kupinduka. Ajali hiyo iliyohusisha basi la kampuni ya NBS yenye makao yake makuu
mjini Tabora, ilitokea saa 3.30 asubuhi nje kidogo ya mji wa Igunga,
mkoani Tabora. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, alisema kuwa chanzo
cha ajali hiyo ni kupasuka kwa gurudumu la mbele la upande wa kushoto
kisha kupinduka. Kamanda Rutta alisema kuwa kati ya waliofariki watatu ni wanawake,
watatu ni wanaume na mtoto mmoja ambaye hata hivyo, jinsia yake
haikujulikana mara moja. Aliwataja waliofariki na kutambuliwa hadi kufikia jana mchana kuwa ni
Zaituni Mziray, Ernesto Iromo, Dickson Nasan na Zainabu Hamud. Kwa mujibu wa Kamanda Rutta, marehemu watatu bado hawajambuliwa majina yao kutokana na kutokuwa na vitambulisho. Alisema kuwa zoezi la kuwatambua linaendelea kufanywa chini ya uangalizi
wa Polisi na kwamba majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Wilaya
ya Igunga. Kamanda Rutta alisema kuwa dereva wa basi hilo lenye namba za usajili T
978 ATM aina ya Scania 94, Idd Hussein Nyohi (33), alinusurika katika
ajali hiyo na ni miongoni mwa majeruhi waliolazwa na kwamba analalamika
kuwa na maumivu makali kifuani. Alisema majeruhi wote wanaendelea vizuri na matibabu na hakuna mwenye
kuhitaji huduma ya rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi hadi sasa. Hata hivyo, Kamanda Rutta alisema bado madaktari wanaendelea kuwafanyia
uchunguzi zaidi majeruhi ili kujua kama kuna madhara zaidi.
No comments:
Post a Comment