Friday, June 15, 2012

Bia yaidhinishwa Brazil Kombe la Dunia 2014

Rais wa Brazil Dilma Rousseff amesaini kuwa sheria muswada utakaoruhusu uuzwaji wa bia wakati wa mechi za Kombe la Dunia mwaka 2014.Shirikisho la Kandanda Duniani, Fifa, lilikuwa linataka mabadiliko katika sheria ya Brazil inayopiga marufuku pombe kuuzwa kwenye mechi za mpira wa miguu. Muswada huo mpya, umeweka sheria kadha kwa ajili ya Kombe la Dunia, haujaelezea kuweka pingamizi lolote la kuuzwa pombe.
Waandishi wa habari wanasema magavana wa majimbo bado wanaweza kupiga marufuku uuzwaji wa bia wakati wa mashindano hayo.
Uuzaji bia umekuwa mwiko katika mechi za kandanda nchini Brazil tangu mwaka 2003.
Upigwaji huo marufuku uliwekwa ikiwa ni sehemu ya hatua ya kupambana na vurugu miongoni mwa mashabiki wa timu zenye uhasama pamoja na kukabiliana na wahuni. Mapema mwaka huu Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke, aliweka bayana kwamba haki ya kuuza bia ni lazima irejeshwe kuwa sheria wakati wa michuano ya Kombe la Dunia kwenye Bunge la Brazil. Wakati wa ziara ya kukagua viwanja kwenye miji 12 ya Brazil itakayochezewa mechi hizo, alionesha hisia zake kwa jambo hilo. "Unywaji wa pombe ni sehemu ya patashika za Kombe la Dunia, kwa hiyo tutahakikisha unaruhusiwa. Mtaniwia radhi iwapo nitakuwa nawakwaza kwa kiasi fulani lakini hilo ni jambo ambalo halina mjadala," alisema. Kampuni ya bia ya Budweiser ndio wadhamini wakubwa wa Fifa.

0 comments:

Post a Comment