Kampuni ya Bia Serengeti (SBL), kwa kushirikiana na Benki ya
NMB, wameichangia timu ya taifa ya soka ya wanawake ''Twiga Stars'' Tshs. Milioni 30
pamoja na vifaa vya michezo, vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 5.5. Mafuru alisema baada ya hivi karibuni kutangaza kudhamini tuzo
za wanamichezo bora za Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA),
walifuatwa na serikali kuombwa kuisaidia Twiga Stars, ambayo haina mdhamini. Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa kuisaidia timu hiyo,
walikutana na NMB, ambao walikuwa wadhamini wenzao katika timu ya soka ya wanaume,
Taifa Stars kabla ya kujitoa mwaka jana, wakakubaliana kuisaidia Twiga kwa
kiwango hicho. Akizungumza katika makabidhiano hayo, yaliyofanyika makao
makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Karume-Ilala, Dar es
Salaam. Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Ephraim Mafuru Balozi alisema kwamba wao
wametoa Sh. Milioni 15 na NMB kiwango kama hicho pia.
Mafuru pia ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza
kuichangia timu hiyo, iliyopo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya
kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika. Kwa upande wake, Meneja Masoko wa NMB, Imani Kajula alisema
kwamba wao kama wadau wakubwa wa michezo wameona umuhimu wa kuisaidia timu hiyo
na pia kuanzisha kampeni ya kuitafutia misaada zaidi. Alisema wamefungua akaunti inayoitwa; Changia Twiga Stars na
amewataka wadau na makampuni mengine kuichangia timu hiyo kupitia akaunti hiyo.
Kajula alisema anaamini kwa sababu benki yao inaongoza kuwa na matawi mengi nchini,
itakuwa rahisi kwa wadau mbalimbali kuisaidia timu hiyo. Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Nasra Juma
Mohamed aliwashukuru SBL na NMB kwa msaada huo na kuahidi matokeo mazuri katika
mechi yao na Ethiopia Mei 27, mwaka huu mjini Addis Ababa. Nasra pia aliwashukuru Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo
na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi walioitembelea
timu hiyo kambini jana Ruvu na kutoa posho ya siku 16 kwa wachezaji na makocha
wa timu hiyo. Nasra amewataka Watanzania kutokatishwa tamaa na matokeo ya timu
hiyo kufungwa mechi mbili mfululizo za
kujipima nguvun dhidi ya Zimbabwe na Afrika Kusini, kwani kupitia mechi hizo
wameweza kubaini mapunfugu ya timu na kuyafanyia kazi na sasa wanaamini timu
iko tayari kuleta matokeo mazuri. Mapema katika Mkutano huo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF,
Sunday Burton Kayuni alisema timu hiyo inakabiliwa na hali mbaya kifedha na kwa
sababu hiyo, TFF ikaamua kusaka wafadhili kwa kushirikiana na serikali na
akawashukuru SBL na NMB kwa kujitokeza. Naye Ofisa wa Wizara ya Habari, Mama Juliana Yassoda, pamoja
na kuwashukuru SBL na NMB, pia ametoa wito kwa makampuni mengine nchini kuiga
mfano wa makampuni hayo kwa kusaidia timu hiyo, ili iweze kufuzu kwa mara ya
pili mfululizo kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika, kwani ina uwezo huo
ikipigwa jeki.
No comments:
Post a Comment